Header Ads


Sober Bagamoyo kwa kushirikiana na Vam -Tz yatarajia kuanzisha Sober ya wanawake

 Naibu waziri wa nishati ambae pia ni Mbunge wa viti maalumu Mkoani Pwani ,Subira Mgalu akipewa taarifa ya mpango wa uanzishwaji wa Sober kwa ajili ya wanawake na wasichana kwa Mratibu wa mpango huo kutoka shirika la Voices of African Mothers Tanzania (VAM-Tz ),Mary Makinda, inayotarajiwa kuanzishwa kwa ushirikiano baina ya Sober Bagamoyo na VAM -Tz .
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
 Vijana waliojikubali katika harakati za kupambana na madawa ya kulevya baada ya kutumia kwa kipindi kirefu bila manufaa kwenye maisha yao na sasa wapo Sober Bagamoyo .
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
 Meneja wa kituo cha Life and Hope Rehabilitation (Sober iliyopo Ukuni Bagamoyo)Godwin Msilu akizungumza kuhusiana na masuala ya madawa ya kulevya katika Jukwaa la wanawake wilayani Bagamoyo.
(Picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo
KITUO cha Life and Hope Rehab (sober Bagamoyo) mkoani Pwani,kwa kushirikiana na Voices of African Mothers Tanzania (VAM-TZ) kinatarajia kuanzisha Sober House ya wanawake itakayowasaidia wanawake na wasichana waliojiingiza kwenye janga la matumizi ya madawa ya kulevya.

Aidha watatoa elimu mbalimbali zitakazowawezesha kuhasi matumizi ya madawa hayo ikiwemo kuachana na tabia hatarishi za uvutaji sigara,unywaji pombe kupita kiasi na kujidunga.

Meneja wa kituo cha Sober Bagamoyo,Godwin Msilu aliyasema hayo wakati akizungumza na wanawake wa jukwaa la uwezeshaji wilayani humo, ambapo Naibu Waziri wa Nishati ,ambae pia ni mbunge wa viti maalum Pwani,Subira Mgalu alishiriki.

Alisema wapo baadhi ya wasichana kwa wanawake waliojiingiza katika utumiaji wa madawa ya kulevya na pombe iliyokithiri lakini hawana mahala pa kukimbilia kupata msaada .

Msilu alisema utumiaji wa madawa ya kulevya una athari kubwa kwa jamii kwani kunasababisha kupata magonjwa ya mapafu,kansa ya mapafu na magonjwa ya moyo.

Alifafanua,matumizi ya sindano za kujidunga zinapelekea kupata maambukizi ya virusi vya ukimwi,maambukizi ya virusi vya homa ya ini (Hepatitis B na C),ambavyo husababisha kudhoofisha afya ya mlengwa.

Msilu aliwaomba akinamama na familia wasichoke kuwaambia ukweli watoto wao kuhusu athari za madawa ya kulevya ,kwani ukishindwa kumlea mtoto kwenye malezi ya awali basi kuna gharama kubwa ya kumrekebisha ukubwani .

 “Tunaanzisha Sober ya wanawake na wasichana wilayani Bagamoyo ,ambayo itatumiwa na kundi hilo na kuleta mabadiliko chanya,tunaamini jumba hilo litawasaidia kwa kiasi kikubwa na kujiona kuwa jamii inawatambua”alisema Msilu.

Akitoa ushuhuda ,Msilu alisema ana umri wa miaka 40 lakini yeye ni mmoja wa waathirika wa madawa hayo ndani ya miaka 20 ya uhai wake .

Alisema alipata bahati ya kusoma na kupata kazi jeshini lakini alipoteza kazi kutokana na kujiingiza kwenye dimbwi la matumizi ya madawa ya kulevya.

Nae mratibu wa mpango huo kutoka VAM –Tz ,Mary Makinda alisema kwa ushirikiano na Sober Bagamoyo watasaidia pia malezi hususan ya wanawake kuanzia utotoni hadi kuvunja ungo ambao hawajapata nafasi hiyo kama wanaume .

Alisema watatoa elimu kwa wazazi ili kuwezesha wazazi waweze kutoa malezi na miongozo ya uwazi inayofaa ili kuwasaidia watoto wao.

“Tutatoa mafunzo kwa vijana kuhusiana na mabadiliko na changamoto zinazowakabili wakati wa makuzi yao”alieleza Mary.

Kwa mujibu wa Mary,watawapa na elimu ya malezi na ujasiriamali,ili kuepuka kujiingiza kwenye makundi hatarishi kwa kufuata maadili ya kitanzania,mila na desturi zinazokubalika kwenye jamii zetu.

Mratibu huyo kutoka VAM-Tz alisema,watahakikisha wale ambao wamepata maambukizi mapya ya ugonjwa wa Ukimwi wanawaunganisha katika huduma za afya ya jamii,kidini na kisaikolojia.

Alibainisha ,ni jukumu lao kuunga mkono juhudi za serikali kusimamia na kufuatilia maisha ya kundi hilo ambalo limeonyesha kupotea na kuliingiza kwenye chuo cha mafunzo (Rehab Centers)na kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ili waweze kuishi maisha mazuri na maadili mema.

Mbunge wa viti maalum mkoani Pwani,Subira Mgalu,aliipongeza Sober Bagamoyo na VAM-Tz kwa kuona umuhimu wa kuanzisha Sober ya wanawake mjini Bagamoyo.

Mgalu aliwataka akinamama kusimamia maadili kuanzia nyumbani ,anasema kazi ya kulinda na kudhibiti watoto ipo mikononi mwao ili kuhakikisha watoto wanakua kwenye makuzi mema.

Alisema serikali ya awamu ya tano inahimiza uchumi wa viwanda na kukuza uwekezaji lakini kama vijana na watoto watakuwa hawana afya njema ,hawataweza kunufaika na matunda hayo.

Mgalu alisema, kiukweli nchi na serikali inajitahidi kuokoa kizazi hicho kuondokana na matumizi ya madawa ya kulevya na kupambana na wanaongiza madawa hayo kwa kuwapa adhabu kali 

No comments

Powered by Blogger.