Dkt. Faustine aviagiza vyombo vya usalama mkoani kigoma kuimarisha mifumo ya udhibiti wa upotevu wa dawa. - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka

Habari za Hivi Punde

Tangaza Hapa +255755300337

Post Top Ad

Post Top Ad


Tuesday, 9 January 2018

Dkt. Faustine aviagiza vyombo vya usalama mkoani kigoma kuimarisha mifumo ya udhibiti wa upotevu wa dawa.

Na.WAMJWW. KIGOMA

Serikali imeviagiza vyombo vya usalama na kamati za Afya za vijiji kuimarisha mifumo yote ya udhibiti wa upotevu wa Dawa nchini, kwa kusimamia na kufuatilia kwa ukaribu hali ya upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, ili kuondoa ubadhilifu unaofanywa na baadhi ya watu wasio waaminifu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (MB) katika ziara yake katika Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma ya kukagua utoaji huduma za Afya na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya jamii ambao unasisitiza ushirikishwaji wa jamii katika maamuzi,

“Niwaombe sana ndugu zangu wananchi tuwe walinzi, hiyo dawa ingeweza kukusaidia wewe, au ndugu yako, hivyo kushiriki katika ubadhilifu huo ni kujiumiza mwenyewe” alisema Dkt. Ndugulile

Katika kupunguza vifo vya kina mama na watoto Dkt. Faustine amesema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewekeza kiasi cha shilingi Milioni 400 katika Halmashauri 175, kikiwemo kituo cha Afya cha Uvinza , fedha zitakazotumika kuboresha na kujenga vyumba vya kutolea huduma ya dharura wakati wa kujifungua, nyumba za watumishi pamoja na maabara.
 
Dkt. Faustine aliendelea kusema kwamba, Serikali inaendelea kufanya vizuri barani Afrika na Dunia kwa ujumla kwa upande wa utoaji chanjo, kwani imefikia asilimia 97 ya walengwa  wote wanaohitaji chanjo nchini jambo linalosaidia kutunza Afya za watu katika jamii.

Dkt. Ndugulile aliongeza kuwa anatambua uhaba wa watumishi unaovikabili vituo vingi vya Afya katika Wilaya ya Uvinza ambao umefikia asilimia 66 na kuahidi kulifanyia kazi ombi hilo ili kupunguza  changamoto katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande mwingine Dkt. Ndugulile ameendelea kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza Bajeti ya dawa , kutoka Bilioni 30 mpaka Bilioni 270 wa mwaka huu wa fedha hali iliyosaidia kuimarisha mapambano dhidi ya maradhi mbali mbali.

Aidha, Dkt. Ndugulile aliwapongeza wananchi wa kata ya Kazuramimba kwa kuonesha kwa vitendo utayari wao wa kusukuma guruduma la maendeleo ya elimu katika Kijiji hicho kwa kuamua kujenga madarasa ya shule katika Kijiji cha Nyanganga kilicha kata ya Kazuramimba ili kuweza kuwakomboa watoto wao na janga la ujinga na umasikini.

Nae Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi Mwanamvua Mlindoko ameeleza faida ya mradi wa ujenzi wa madarasa ikiwemo ongezeko la ufaulu kutoka wanafunzi 4115  mwaka 2017 huku waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza ni wanafunzi 1641 ambao ni sawa na asilimia 36 tu, hivyo kutokana na ujenzi wa madarasa haya utasaidia wanafunzi 2482 sawa na asilimia 64 kuendelea na elimu.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akihesabu harambee ndogo aliyoiongoza pindi alipofanya ziara yake katika kata ya Kazuramimba, harambee hiyo itasaidia katika jitihada za kuendeleza ujenzi wa madarasa hayo, katikati ni Mkuu wa Wilaya ya Uvinza Bi. Mwanamvua Mlindoko
 Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akiongea na wazazi juu ya umuhimu wa virutubisho vilivyo kwa mama pindi ananyonyesha katika eneo la kupokea chanjo kwa watoto walio na umri chini ya miaka 5
 Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua nembo ya MSD GOT katika dawa inayoonesha kuwa dawa hiyo imetolewa na Serikali na haipaswi kuuzwa
 Kundi la wanakijiji wa kata ya Kazuramimba waliojitokeza kumsikiliza Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile pindi alipofanya ziara katika Kata ya Kazuramimba kujionea ujenzi wa Madarasa ya shule.
 Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akifuatilia majibu ya mama mjamzito kuhusu upatikanaji bure wa vifaa vya kujifungulia, kushoto ni Mkurugenzi wa Wilaya ya Kasulu Dkt Dastan.
Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akisalimiana na mmoja kati ya wagonjwa katika Hospitali ya Kasulu Mkoani Kigoma

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Tangaza Hapa +255755300337