Header Ads


Waziri Mhe Mpina amtaka Mwekezaji kuondoka mara moja

Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Mh.Luhaga Mpina  (katikati) kitoa maamuzi ya kuitaka Kampuni ya Game Tracking Safaris(TGTS)  kuondoka katika eneo la hekta 20000 kwenye vitalu  tisa vilivyomo kwenye Ranchi  ya Uvinza ifikapo tarehe 1/1/2018.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mh. Luhaga Mpina  ameutaka uongozi wa  Kampuni ya Game Tracking Safaris(TGTS)  kuangalia na kupitia nyaraka walizonazo  ili kuona uhalali wa umiliki wa eneo la hekta 20000 kwenye vitalu  tisa vilivyomo kwenye Ranchi ya Uvinza inayomilikiwa na  Kampuni ya Ranchi za za Mifugo za Taifa (NARCO)kabla ya Selikali kuwatoa kwa nguvu ifikapo tarehe 1/1/2018.

 Waziri Mpina ametoa maelekezo  hayo leo alipotembelea Ranchi ya Uvinza kuangalia shughuli mbalimbali  katika Ranchi hiyo ambapo ametoa muda wa hadi Januari mosi mwakani  kwa mwekezaji huyo kuondoka katika eneo hilo  endapo atabaini kuwa amekuwa akikaa kimakosa kuanzia katika  vitalu namba 41 hadi 49.

Aidha Waziri Mpina amesema  endapo Mwekezaji huyo ataendelea kubaki  baada ya tarehe Mosi Januari, Serikali itamuondoa kwa nguvu  na atatakiwa kulipa gharama  zote za fidia na usumbufu.

 “Ninakuagiza  angalia  taarifa  mbalimbali ulizonazo kuhusu  umiliki wa eneo hili kama utaona  umeendelea  kukaa  hapa  bila kufuata taratibu tafadhali  uondoke mara mmoja ili kupisha Serikali kuendelea na shughuli zake” alisisitiza Mpina

Waziri Mpina  amemuagiza Meneja Mkuu wa NARCO, Profesa  Philemoni Wambura  kuwaandikia  barua  ya kuwaondoa wawekezaji wote katika Ranchi hiyo ambao hawajaendeleza kwa zaidi ya asilimia 40  na kwamba wawekezaji ambao wamewekeza kwa zaidi ya asilimia arobaini wanatakiwa kukamilisha malipo yote kabla ya Januari mosi mwakani.

Alionya wawekezaji kuacha tabia ya kuidanganya serikali kwamba wanauwezo wa kuwekeza katika vitalu  ili wapewe lakini wanabadili matumizi baada ya kupewa. 

Aliongeza kwamba  Serikali imegundua  baadhi ya wawekezaji wanaopewa vitalu wanawakodisha wafugaji kutoka nchi jirani  na kujipatia faida wakati  Serikali haipati chochote.


Awali, Meneja wa (TGTS)   Audax Kalulama  akizungumza kwa simu  na Waziri Mpina kutoka Arusha amesema kwamba  eneo hilo wanamiliki  kihalali na kuomba muda ili wawasiliane na Wizara  ya Mifugo kuonyesha  taarifa  za umiliki wa eneo hilo.

No comments

Powered by Blogger.