Wanafunzi 1,300 wa s/m na sekondari pwani waacha shule 2014/2017 - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka

Habari za Hivi Punde

Tangaza Hapa +255755300337

Post Top Ad

Post Top Ad


Thursday, 21 December 2017

Wanafunzi 1,300 wa s/m na sekondari pwani waacha shule 2014/2017

 Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, akizungumza jambo kuhusu masuala ya sekta ya elimu na changamoto inazozikabili kwa viongozi na wadau mbalimbali wa elimu mkoani hapo kwenye ukumbi wa mikutano katika ofisi za jengo la mkuu wa mkoa .  (Picha na Mwamvua Mwinyi)
Baadhi ya viongozi na wadau wa elimu mkoani Pwani wakimsikiliza mkuu wa mkoa huo mhandisi Evarist Ndikilo ,wakati alipokuwa akizungumza masuala ya elimu na changamoto zinaxokabili sekta hiyo ,kwenye ukumbi wa mikutano uliopo katika ofisi ya mkuu wa mkoa wa Pwani.

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

SERIKALI mkoani Pwani ,imeweka bayana kuwa,jumla ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari 1,300 wameacha shule (mdondoko),kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2014-2017,hali inayosababisha kukosa haki yao ya elimu.

Aidha kumekuwa na tetesi kwamba baadhi ya watoto hao wanaoacha shule hujihusisha na vikundi vya uhalifu ndani na nje ya mkoa huo ,jambo ambalo linahitaji nguvu za pamoja kulikomesha tatizo hilo.

Pamoja na hilo ,imeeleza kumekuwepo na tatizo la uzembe kwa baadhi ya wasimamizi wa elimu kutotekeleza ipasavyo majukumu yao,;:na pia kutofikiwa kwa malengo ya uandikishaji wa elimu ya awali na darasa la kwanza na udahili wa kidato cha kwanza hivyo kusababisha watoto wenye umri wa kwenda shule kutokwenda shule.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,aliyasema hayo wakati akizungumzia changamoto na masuala ya sekta ya elimu mkoa,kwa viongozi wa Idara ya elimu mkoani hapo, wakurugenzi,wakuu wa wilaya na wadau wa elimu.

Alielezea ,kati ya watoto hao 1,300 wanaodaiwa kuacha shule kwenye mkoa mzima ,kwa upande wa wilaya ya Rufiji ni wanafunzi 381 na Kibiti ni 110 .

"Niliwahi kuomba taarifa ya mdondoko kwa kipindi cha mwaka 2014-2017 kutoka kwa wakuu wa wilaya zote "

"Ambapo mkoa wa Pwani una jumla ya shule za msingi 613 na sekondari 174 ,ndipo nilipoletewa idadi hiyo ambayo kiukweli ni chanzo cha kuporomoko  kwa taaluma mkoani hapo" alisema mhandisi Ndikilo.

Mhandisi Ndikilo aliagiza wanafunzi wote walioacha shule na watoro watafutwe ,warudishwe shule kisha wazazi na walezi wachukuliwe hatua za kisheria ikiwepo kufikishwa mahakamani kwa kushindwa kufuatilia mahudhurio ya watoto hao.

Alibainisha lipo tatizo jingine la mimba kwa watoto wa kike ,upungufu na uchakavu wa miundombinu ya shule ikiwemo madarasa ,nyumba za walimu ,matundu ya vyoo,ofisi za walimu, maabara na hostel.

Mkuu huyo wa mkoa, alisema kwasasa shule za msingi kuna mahitaji ya vyumba vya madarasa 7,609 ,vilivyopo ni 4,010 hivyo upungufu ni madarasa 3,599.

Mahitaji ya nyumba za walimu ni 6,328 ,zilizopo ni 1,592 ,upungufu ni nyumba 4,736 ,matundu ya vyoo yanayohitajika ni 13,750 ,yaliyopo ni 5,375 upungufu ni matundu 8,375 .

Mhandisi Ndikilo alitaja mahitaji ya vyumba vya madarasa katika shule za sekondari mkoani Pwani kuwa ni 1,479 ,vilivyopo ni 1,366 ,upungufu ni 113 ,mahitaji ya nyumba za walimu 3,684 zilizopo 671 hivyo upungufu 3,013.

Matundu ya vyoo yanayohitajika ni 2,405 yaliyopo ni matundu 1,961,upungufu ni matundu 444 ,na mahitaji ya maabara ni 333 yaliyopo ni 195 na upungufu ni 138.

Hata hivyo ,Mhandisi Ndikilo alizitaka halmashauri mkoani humo ,ziande mkakati wa kujenga hostel katika kila shule ya sekondari ili kuwalinda watoto hasa wa kike wanaotembea umbali mrefu kwenda na kurudi shule.

Sanjali na hilo ,ziwe na mpango mkakati wa kujenga na kukarabati miundombinu ya shule ikiwemo vyumba vya madarasa ,matundu ya vyoo na nyumba za walimu na kukamilisha ujenzi ifikapo 2020 .

Alitoa wito kwa wadau wa elimu kuunga mkono juhudi za serikali ya mkoa katika ujenzi wa miundombinu katika shule za msingi na sekondari.

Katika hatua nyingine ,mhandisi Ndikilo alisema lengo la serikali ni kuimarisha sera ya viwanda ili kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025 ,na msingi mkubwa wa sera hiyo ni elimu.

Aliwataka wakuu wa wilaya, wakurugenzi, watendaji wa halmashauri pamoja na watendaji wengine kuhakikisha wanafunzi wanaodahiliwa kidato cha kwanza wanasimamiwa hadi wanamaliza kidato cha nne ili waweze kushiriki katika kuimarisha uchumi wa viwanda.

Alisema kwamba,watoto wasipopewa elimu ,maarifa na ujuzi mahsusi watakuwa watazamaji badala ya watendaji licha ya mkoa huo kusheheni viwanda.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Tangaza Hapa +255755300337