Header Ads


Wakulima wataka pamba yao inunuliwe kwa fedha tasilimu.

Na Tiganya Vincent
RS-Tabora

BAADHI ya wakulima wa Pamba wilayani Nzega wameiomba Serikali kudhibiti mtindo wa Kampuni ambazo zimekuwa na tabia ya kukopa mazao ya wakulima kwani vitendo hivyo vimekuwa vikiwakatisha tamaa.

Kauli hiyo ilitolewa jana Wilayani Nzega na baadhi ya wakulima wakati wa Mkutano na Mkuu wa Tabora Aggrey Mwanri alipokuwa katika ziara ya kukagua mashamba ya pamba katika kwenye maeneo ili kujionea kama wamezingatia kanuni za kilimo cha zao hilo.

Mkazi wa Kitongoji cha Ihange katika Kata ya Ndala Fidelis Francis alisema kuwa katika kipindi cha nyuma wakulima wengi wa pamba walikatwishwa tamaa na wanunuzi ambao walichukua pamba yao na kulipa baadhi ya wakulima wachache na waliobaki kuambiwa watalipwa siku ya baadaye.

Alisema kuwa vitendo vya aina hiyo ndio walivyopelekea baadhi yao kuachana na kilimo cha pamba na kujikita katika kulima mazao mengine ili kupata fedha za kuendeshea maisha yao na familia.

Naye Elias Mwabila alisema kuwa baadhi ya wakulima walikuwa wakitumia mapato ya zao hilo kwa ajili ya kununulia chakula na malipo kwa ajili ya ada watoto wao na kununua mahitaji mengine muhimu ikiwemo mifugo na vifaa vya ujenzi.

Alisema kuwa  kitendo cha kukopa pamba yao kiliwafanya waishi maisha ya shida na  kuwasababisha kutoona tena umuhimu wa zao hilo.

Akijibu hoja za Wakulima hao Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mwanri alisema kuwa katika msimu huu mfumo utakaotumika kununua pamba mkoani humo ni wa papo kwa papo , hakuna cha kusubiri hadi siku nyngine.

Alisema kuwa Kampuni zote zilizopewa jukumu la ununuzi wa pamba katika Mkoa wa Tabora ni vema zihakikishe zimejiandaa kikamilifu na kuwa na fedha za kutosha kwani hawezi kukubali pamba ya wakulima ichukuliwe kwa mkopo.

Mwanri alisema kuwa uongozi wa Mkoa wa Tabora umejipanga kuhakikiha kuwa unamshika mkono mkulima katika hatua zote na utamwachia mkono akishalipwa pesa zake kwa ajili ya kwenda kujipangia matumizi.

Alisema kuwa hawezi kuona wakulima wakiendelea kuuza mazao yao kwa mkopo hatua ambayo ndio imekuwa ikichangia kuuza zao hilo na vyama vya msingi na hivyo kuikosesha Serikali mapato.

No comments

Powered by Blogger.