Wakazi wa Tabora wavutia na kampeni za upandaji wa miti - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka

Habari za Hivi Punde

Tangaza Hapa +255755300337

Post Top Ad

Post Top Ad


Wednesday, 13 December 2017

Wakazi wa Tabora wavutia na kampeni za upandaji wa miti

NA TIGANYA VINCENT -RS TABORA

UAMUZI wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri kuagiza Halmashauri zote kuhakikisha zinapanda wa miti ya matunda katika shule na taasisi umepongezwa na wakazi mbalimbali mkoani humo kwa kuwa utawasaidia kuimarisha afya zao.

Wakazi hao walitoa pongezi hizo jana mjini Tabora wakati Mkuu huyo Mkoa alipokuwa akizundua zoezi la upandaji wa miti ya matunda ya michungwa na mipapai katika barabara ya kwenda Nzega kutoka Manispaa ya Tabora.

Mmoja wa wakazi hao ambaye ni Mfanyabiashara katika Soko Kuu Tabora Athuman Maango alisema kuwa hatua ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kuagiza upandaji wa miti aina mbalimbali ya matunda katika maeneo ya Hospitali, Shule, nyumba za ibada ni cha kuungwa mkono kwa nguvu zote kwani kinalenga kujenga afya za wakazi wa eneo hilo.

Alisema kuwa matunda yakipatikana kwa wingi watoto wakula na kuwa na afya njema na ziada yatauzwa kwa ajili ya kuongeza kipato cha wahusika.

Maango alisema kuwa watakuwa walinzi wa miti hiyo ya matunda na mingine ili watu wenye tabia ya kuchoma moto ovyo na wanyama wasiweze kuiharibu na kukatisha ndoto za Mkuu wa Mkoa wa Tabora za kutaka kugeuza Mkoa huo kuwa wa kijani.

Mkazi mwingine ambaye ni Mwenyekiti wa Tabora Transport Motorcycle Kassim Kidulu alisema kuwa kampeni ya Mkuu wa Mkoa ya upandaji wa matunda katika maeneo mbalimbali inatarajia kurejesha heshima ya eneo hilo kuwa miongoni mwa wazalishaji wa matunda hasa maembe.

Alisema kuwa heshima hiyo imeanza kupotea kutokana na  baadhi ya watu kukata miti ya miembe na mipera katika maeneo mbalimabli kama vile Ipuli katika Manispaa ya Tabora kwa ajili ya kuchomea tofauli na kwa maeneo mengine kuchomea tumbaku.

Kidulu aliongeza kuwa enzi za nyuma watoto walikuwa wakienda kuchuma mapera na maembe katika eneo la Ipuli , lakini hivi hakuna kwa sababu ya ubinafsi wa baadhi ya watu kuangalia maslahi yao na sio maslahi mapana ya jamii.

“Mkuu wa Mkoa kitendo ulikionyesha cha kuanza kupanda matunda katika Mkoa wetu kimenifurahisha sana na ni cha kuigwa ...kwani embeo tunazokula hivi sasa nyingi zilipandwa na babu zetu , bila wao hizi hazingekuwepo…kwa hiyo kitu ulichoanzisha sisi tunakiunga mkono na utapata thawabu kwa Mungu” alisema Kidulu.

Naye Mamalishe katika barabara ya Sikonge Pili Said alisema kuwa ataendelea kuunga mkono juhudi za Mkuu huyo wa Mkoa ili hatimaye Tabora iwe ya kijani kama ilivyo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Naye Msaidizi Askofu wa Dayosisi ya Magharibi Kati Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Newton Maganga alisema kuwa kitendo alichokianzisha Mkuu wa Mkoa ni kuendeleza kazi ya Mungu wakati aliwaumba Adamu na Hawa na kuwaweka katika bustani ya Edeni.

Akizindua upandaji wa miti ya matunda na miti mingine katika Manispaa ya Tabora Mwanri alisema kuwa kutakuwa na upandaji wa miti ya matunda katika taasisi zote za dini, mashuleni, hospitali, mitaani na wananchi watahimizwa kwa ajili ya kupanda miti hiyo.

Alisema kuwa matunda yakizalishwa kwa wingi upo uwezekano mkubwa kuwavutia wawekezaji wakubwa kuanzisha kiwanda cha kusindika kwa kuwa kutakuwepo na malighafi za kutosha na hivyo wananchi kupata pesa baada ya kuwauzia wawekezaji hao.

Kampeni hiyo ilianza katika Wilaya mbalimbali inalenga kupanda miti ya matunda 6000 kila Halmashauri na miti miwili kwa kila familia na miti mingine ikiwa sehemu ya kutaka kuifanya Tabora kuwa kijani.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Tangaza Hapa +255755300337