Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini Watakiwa kujiunga kwenye vikundi - Mtazamo News
Tangaza Biashara yako Hapa +255755 300 337

HABARI ZA HIVI PUNDE

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Sunday, 3 December 2017

Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini Watakiwa kujiunga kwenye vikundi

Wachimbaji Wadogo wa Madini nchini wamesisitizwa kujiunga kwenye vikundi ili iwe rahisi kusaidiwa.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ametoa wito huo Desemba 2, 2017 Wilayani Ruangwa kwenye mkutano wake na wachimbaji wadogo wa madini ya Dhahabu na Vito (Green Garnet) wa Namungo wilayani humo. 

Nyongo alisema dhamira ya Serikali ni kuwasaidia wachimbaji wadogo kuwa na uchimbaji wenye manufaa kwao na kwa Taifa kwa ujumla na ili kufikia dhamira hiyo ni vyema wakajiunga kwenye makundi.

"Mkijiunga kwenye makundi itakua ni rahisi kuwapatia misaada mbalimbali yenye tija kwenye shughuli zenu," alisema.

Alisisitiza kwamba daima umoja ni nguvu, na ili mchimbaji awe na uwezo na nguvu kwenye utekelezaji wa majukumu yake inabidi afanye kazi akiwa ndani ya umoja na wenzake.

Alisema pale ambapo wachimbaji watakua wamejiunga kwenye makundi, itakua rahisi hata kwa Taasisi za kifedha kuweza kuwafikia na kuwasaidia.

"Nimekuja hapa kuzungumza nanyi ili kubaini changamoto zinazowakabili kwa ajili ya kuzitafutia ufumbuzi, ninawaasa mhakikishe mnajiunga kwenye vikundi," alisema.

Aliongeza kwamba Serikali ingependa kuona Wachimbaji Wadogo wa Madini wanafanikiwa kufikia kwenye uchimbaji wa Kati na baadaye kuwa Wachimbaji Wakubwa.

Aidha, Wachimbaji hao walimuomba Naibu Waziri Nyongo kuendelea kuwatembelea mara kwa mara ili kuelewa changamoto zinazowakabili na kuzifanyia kazi kila inapobidi.

Baada ya kuzungumza na wachimbaji hao, Naibu Waziri Nyongo alitembelea Mgodi wa Dhahabu unaomilikiwa na Kampuni ya Germin Exploration ya Namungo huko Ruangwa na kukagua shughuli zinazofanywa na mgodi huo.

Vilevile alitembelea mradi wa kuchimba madini ya kinywe (graphite) wa Kampuni ya PACCO GEMS LTD iliyopo katika kijiji cha Mtondo na Nanjaru wilayani humo ambapo  aliahidi kuwasaidia kumaliza tatizo la upatikanaji wa hati ya umiliki wa ardhi wanayohitaji ili mradi uweze kuanza mara moja.

Naibu Waziri Nyongo yupo Mkoani Lindi kwa ajili ya ziara ya kutembelea Miradi ya Madini pamoja na kuzungumza na wachimbaji kwa lengo la kuwekeana mikakati ya kuwa na uchimbaji wenye tija kwao na Taifa kwa ujumla.
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akipata maelezo ya mradi wa kuchimba madini ya kinywe (graphite) wa Kampuni ya PACCO GEMS LTD iliyopo katika kijiji cha Mtondo na Nanjaru wilayani humo 
 Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo alipotembelea na kuzungumza na Wachimbaji kwenye Miradi ya kuchimba Madini ya Dhahabu na Kinywe Wilayani Ruangwa

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages