Naibu Waziri Mgalu awataka wakandarasi Tanga kutoa maelezo ya kutokuanza miradi - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka

Habari za Hivi Punde

Tangaza Hapa +255755300337

Post Top Ad

Post Top Ad


Sunday, 17 December 2017

Naibu Waziri Mgalu awataka wakandarasi Tanga kutoa maelezo ya kutokuanza miradi

 Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akifafanua jambo mbele ya wanakijiji wa kijiji cha Mbuluni wilayani Mkinga mkoani Tanga (hawapo pichani) katika mkutano wa hadhara.
Sehemu ya wakazi wa kijiji cha Mtindiro kilichopo Muheza mkoani Tanga wakifuatilia hotuba iliyokuwa inatolewa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu (hayupo pichani)

Na Greyson Mwase, Tanga

Naibu Waziri wa Nishati,  Subira Mgalu amezitaka kampuni za  Derm Electric, Njarita, Agwilla na  Radi Services kutoa maelezo  kupitia  Wakala wa Nishati  Vijijini (REA) ya kutokuendelea na kazi katika maeneo yao ya miradi wakati walikwishalipwa malipo ya awali na  Serikali.

Mgalu alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki tarehe 16 Desemba, 2017 alipofanya kikao na watendaji wa Shirika la  Umeme  Tanzania (TANESCO)- Ofisi ya Tanga baada ya kubaini wakandarasi hao hawapo katika maeneo hayo ya kazi na kutohudhuria kikao hicho kama alivyoagiza.

Kikao hicho kilishirikisha pia watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Wakala wa Nishati Vijijini (REA)

Alisema kitendo cha  wakandarasi kutokuwepo katika maeneo yao ya kazi na kutohudhuria kikao kama ilivyoagizwa kinakwamisha utekelezaji wa miradi na hivyo kuutaka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kujulisha kampuni husika kuandika maelezo ya kutokuwepo kwenye  maeneo ya kazi na kukwamisha juhudi za  Serikali katika usambazaji wa umeme vijijini.

“ Kama Serikali tumeweka mikakati ya kuhakikisha ifikapo mwaka 2019- 2021 vijiji vyote nchini vinafikiwa na huduma ya umeme, sasa inapotokea baadhi ya wakandarasi wanakwamisha  juhudi hizi wakati wamekwishalipwa na Serikali ni lazima Serikali iwawajibishe kulingana na sheria na kanuni za nchi,” alisema Mgalu.

Mgalu aliendelea  kuwataka wakandarasi wote nchini  kuwepo katika maeneo yao ya kazi na kukamilisha miradi yao kwa wakati, na kusisitiza kuwa serikali  haitamvumilia mkandarasi yeyote atakayefanya kazi katika kiwango cha chini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mgalu aliitaka TANESCO kuwa wabunifu kwenye ukusanyaji wa madeni  na kukamilisha zoezi la  uhakiki wa wateja mara moja ili kukabiliana na changamoto ya upotevu wa mapato ya shirika hilo.

Alisema ni jukumu la TANESCO kujiendesha kwa faida kupitia mapato yake na kazi ya Serikali ni kulipa nguvu shirika hilo kwa miradi mikubwa inayohitaji fedha nyingi.

Wakati huo huo, akizungumza katika mikutano tofauti katika kijiji cha Zangibari kilichopo wilayani Mkinga na katika vijiji vya Mlingano,  Mtindiro, Mpapayu vilivyopo katika wilaya ya Muheza mkoani Tanga, Naibu Waziri Mgalu alielekeza wakati wa utekelezaji wa miradi, Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) kuhakikisha taasisi, shule, nyumba za ibada, hospitali zinapata umeme.

Aidha  alipongeza wananchi wengi  katika vijiji vya Zangibari wilayani Mkinga na  Mpapayu wilayani Muheza mkoani Tanga  walioonyesha mwitikio mkubwa wa kuunganisha mfumo wa umeme ( wiring) kwenye nyumba zao na kuwataka ambao hawajaunganisha mfumo wa umeme kufanya mara moja kwa ajili ya neema kubwa ya umeme.

Alisema kwa wale ambao wana nyumba ndogo wanaweza kuwekewa kifaa maalum cha Umeme Tayari (UMETA) na kuanza kufaidi huduma ya umeme.

Akielezea mikakati ya serikali katika uboreshaji wa upatikanaji wa umeme wa uhakika na kwa gharama nafuu, Mgalu alisema kuwa serikali kupitia REA Awamu ya Tatu  inasambaza umeme katika vijiji vyote nchini ambapo  ifikapo mwaka 2019 karibia vijiji vyote vitakuwa na umeme wa uhakika.

Aliendelea kuelezea mikakati mingine kuwa ni pamoja na matumizi ya nishati  jadidifu kama vile jua hususan katika maeneo yasiyofikiwa na umeme kutoka Gridi ya Taifa, ujenzi wa  mradi  wa kuzalisha umeme  kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto  Rufiji wa Stieglers Gorge na mradi wa kuzalisha  umeme kwa kutumia  gesi asilia wa Kinyerezi I na Kinyerezi II.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Tangaza Hapa +255755300337