Header Ads


Mwenyekiti wa CCM Pwani asema wapinzani hawana safari 2019-2020

 Mwakilishi mkutano mkuu wa mkoa wa Pwani ,Imani Madega, akizungumza kwenye sherehe za kupongezwa kuchaguliwa kwa uongozi Mpya wa CCM Mkoani hapo ,iliyoandaliwa na CCM kata ya Bwilingu jimbo la Chalinze.
(Mwamvua Mwinyi
Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi (CCM)Mkoani Pwani Ramadhan Maneno ,akizungumza kwenye sherehe za kumpongeza kushika nyadhifa hiyo ,iliyoandaliwa na CCM kata ya Bwilingu jimbo la Chalinze.
(Mwamvua Mwinyi)

Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze

MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno amesema, atahakikisha anakomboa maeneo mbalimbali yanayoongozwa na vyama vya upinzani mkoani humo katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Aidha amewataka wanaccm kuachana na siasa za mazoea ambazo zimekuwa zikikiumiza chama hasa nyakati za uchaguzi ambapo husababisha wanachama kuwapigia kura wapinzani na kukikandamiza chama.

Aliyasema hayo Chalinze wakati wa sherehe za kumpongeza kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo   zilizoandaliwa na Ccm kata ya Bwilingu.

Maneno alieleza kwa kushirikiana wanaCCm na kujenga umoja kwa hakika ushindi utapatikana na kurejesha maeneo yaliyopotezwa kwenye uchaguzi uliopita.

Alisema yeye na viongozi waliochaguliwa wana kazi kubwa ya kukiimarisha chama na kuendelea kushika dola.

"Kuna kata, vitongoji, vijiji na mitaa vinashikiliwa na upinzani ambapo waliongoza wakati wa chaguzi zilizopita,ni lazima tuzirudishe "

“Tunaimani tutavirudisha kwenye himaya yetu na kutokana na yanayofanywa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Magufuli kwa sasa wapinzani hawana safari na kata 28, mitaa 11, vitongoji 38 na vijiji 76 ambavyo vinashikiliwa na wapinzani mkoa mzima tutavikomboa,” alisema Maneno.

Alielezea ili kufanikiwa kwenye hilo wataanza mikakati mapema kwa kuhakikisha wanaweka wagombea ambao wana uwezo na si kwa upendeleo na malumbano ambayo yanasababisha kutoelewana.

“Kikubwa ni kuhakikisha tunamsaidia Rais kwani yeye tayari kaanzisha njia tukifuata anavyotaka hatutapata taabu na tusisubiri hadi dakika za mwisho kama kuna mtu anakikwamisha chama ni vema kumsema na si kumficha na tuangalie tulijikwaa wapi ,” alisema Maneno.

Akizungumzia kuhusu siasa za mazoea alisema zimekiharibu chama kwa watu kushindwa kuwakemea wale wanaokwenda kinyume na katiba ya chama na kujiona kuwa wao ni miungu watu .

Alisema siasa za namna hiyo ni za kuumizana kama mtu kakosea asemwe kwenye vikao husika .

Awali akimkaribisha mwenyekiti mwakilishi mkutano mkuu wa mkoa Imani Madega, aliwataka wanaCCM waondoe makundi na kurekebishana pale penye makosa.

Madega alisema makundi ni moja ya chanzo kinachosababisha kushindwa kwenye chaguzi mbalimbali dhidi ya wapinzani.

Nae mwenyekiti wa halmashauri Saidi Zikatimu alisema  atahakikisha anakaa na madiwani ili kuondoa changamoto zilizopo ambazo zimeonekana baina ya madiwani wa halmashauri hiyo mpya ya Chalinze.

Zikatimu aliomba wawe kitu kimoja pia wao kama madiwani watahakikisha wanaisimamia serikali ili iweze kutekeleza ilani ya chama ambayo ndiyo inayoongoza nchi kwa sasa.

No comments

Powered by Blogger.