Kawambwa atoa mil.15.4 kwa vikundi 26 kupitia mfuko wa jimbo la Bagamoyo - Mtazamo News
Tangaza Biashara yako Hapa +255755 300 337

HABARI ZA HIVI PUNDE

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Friday, 3 November 2017

Kawambwa atoa mil.15.4 kwa vikundi 26 kupitia mfuko wa jimbo la Bagamoyo

 Akikabidhi hundi kwa niaba ya mbunge wa Bagamoyo Shukuru Kawambwa  kwa viongozi wa vikundi 26 katika jimbo hilo,makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ,Saidi Ngatipula ,wakati wa hafla fupi ya kukabidhi fedha mil.15.400 zilizotokana na mfuko wa jimbo .
 Mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo ,Fatuma Latu,akisema neno wakati wa hafla fupi ya kukabidhi fedha mil.15.400 kwa vikundi 26 jimboni hapo kupitia mfuko wa jimbo .
Katibu wa Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Magreth Masenga akizungumza jambo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi fedha mil.15.400 kwa vikundi 26 jimboni hapo kupitia mfuko wa jimbo .

(Picha na Mwamvua Mwinyi)
.....
Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

VIKUNDI vya ujasiriamali pamoja na taasisi vipatavyo 26 katika jimbo la Bagamoyo Mkoani Pwani vimewezeshwa sh.milioni 15.400 kupitia mfuko wa jimbo hilo ili kujiinua kimaendeleo.

Aidha vikundi hivyo vimetakiwa kutumia fedha hizo kwa matumizi lengwa badala ya kunywea pombe na kufanyia mikogo kwenye nyumba ndogo.

Akizungumza wakati akikabidhi hundi kwa niaba ya mbunge wa Bagamoyo Shukuru Kawambwa  kwa viongozi wa makundi hayo ,makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo ,Saidi Ngatipula ,alisema endapo fedha hizo zikitumika vizuri zinasaidia na kuondoa umasikini.

Ngatipula ambae pia ni mjumbe wa kamati ya mfuko huo wa jimbo ,alielezea ,fedha za mfuko wa jimbo ni ndogo lakini zina manufaa kwa wale wanaozipangia mipango yenye tija .

"Wapo wanaojinasibu kuwa pochi la mbunge limemuanguka wakiokota basi ,hiyo sio kauli yenye hekima kwani unaweza kuokota hilo pochi na kufanyia mambo ya maana" alisema Ngatipula.

Alimpongeza mbunge Kawambwa kwa ushirikiano wake na halmashauri kwa kuhakikisha wanasukuma maendeleo katika jimbo na kuwezesha makundi maalum kupitia mfuko wa jimbo na wakati mwingine fedha zake binafsi .

Nae Mkurugenzi wa halmashauri ya Bagamoyo ,Fatuma Latu alisema mwaka 2016-2017 halmashauri hiyo ilitoa mapato yake ya ndani kwa asilimia 100 na kuwezesha asilimia 5 kwa wanawake na asilimia 5 vijana.

Alieleza kipindi cha nyuma wananchi walijua fedha zinazotolewa na serikali ni ya bure hivyo kusababisha urejeshaji wa mikopo kutokuwa mzuri .

Fatuma alisema kwasasa wanatoa elimu ya kutosha na wanashukuru urejeshaji upo vizuri na wanavifuatilia  vikundi vyote wanavyovipatia fedha ili kujua kama wanazitumia kwa matumizi lengwa.

Kwa upande wake katibu wa Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Magreth Masenga alibainisha  licha ya kutolewa kwa fedha za jimbo lakini Kawambwa anaendelea kusimamia changamoto mbalimbali zinazowakabili wana Bagamoyo ikiwemo elimu ,afya,miundombinu na kusaidia makundi maalum .

Alisema ili kuhakikisha vikundi vyote vinanufaika wanavifuatilia na kutembelea vikundi vinavyopatiwa fedha,ambapo juzi walikuwa katika ziara ya siku tatu ya kufuatilia na kutembelea miradi wanayoifanya wanakikundi hao.

Magreth aliviomba vikundi hivyo vitumie vizuri fedha hizo na kurejesha kwa wakati ili ziweze kunufaisha wengine ambao bado hawajafanikiwa .

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages