Dk.Kawambwa ashirikiana na wafadhili uchimbaji wa visima 30 vilivyogharimu mil.240 jimboni Bagamoyo - Mtazamo News
Tangaza Biashara yako Hapa +255755 300 337

HABARI ZA HIVI PUNDE

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Tuesday, 21 November 2017

Dk.Kawambwa ashirikiana na wafadhili uchimbaji wa visima 30 vilivyogharimu mil.240 jimboni Bagamoyo

Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo

MBUNGE wa jimbo la Bagamoyo ,Dk.Shukuru Kawambwa ameshirikiana na wafadhili mbalimbali kuwezesha uchimbaji wa visima 30 vilivyogharimu kiasi cha sh.mil.240 jimboni humo.

Aidha amechangia sh.mil.mbili na mifuko 70 ya saruji kwenye ujenzi wa zahanati ya kitongoji cha Kimara Ng'ombe Kata ya Nianjema.

Dk.Kawambwa aliyaeleza hayo,wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea miradi ya maendeleo ya kijamii ikiwemo miundombinu ya madarasa,ofisi za walimu,zahanati,kilimo,maji,vikundi vya ujasiariamali kwenye kata ya Nianjema ambapo aliambatana na kamati ya siasa ya CCM ya kata hiyo .

Alisema kati ya visima hivyo 30 vilivyochimbwa visima vitano vipo katika kata hiyo.

Dk.Kawambwa alisema anaendelea na juhudi za kuomba wahisani ambapo kwasasa wanashirikiana na taasisi ya Time To Help na Rehema Friendship kutoka Uturuki ambao wamesaidia kuchimbwa kwa visima hivyo.

Alielezea visima vitapunguza makali na adha kwa wananchi na akinamama ambao wanapata shida ya kufuata maji umbali mrefu na kudamka alfajiri kwenda kuchota maji.

"Tukiendelea kusubiri kukamilika mradi mkubwa wa maji wa WAMI awamu ya tatu  ,sisi tuna bahati kwani maeneo mengi jimboni hapa yana maji chini ya ardhi,kikubwa ni kuweza kuchimba na kuweka miundombinu ili kupata maji"aliongeza Dk.Kawambwa.

Akizungumzia juu ya ujenzi wa zahanati ya Kimara Ng'ombe alisema amefikishiwa taarifa kuwa halmashauri umesitisha kutoa ahadi yake ya mil.10 ilizoahidi .

Dk.Kawambwa aliahidi kuzungumza na halmashauri kupitia mganga mkuu wa wilaya ya Bagamoyo kujua changamoto iliyosababisha kukwama kwa ahadi na ujenzi huo.

Alisema kwamba,kukamilika kwa zahanati  hiyo kungesaidia kuondoa tatizo la kufuata huduma za afya mbali na eneo husika.

"Wananchi wamekuwa wakitumia nguvu kazi na kuchangia,na madiwani nimekuwa nikishirikiana nao kutekeleza miradi hiyo huku wafadhili wakiwa wamesaidia kutushika mkono"

"Nimefanya katika kipindi cha miaka miwili tangu nichaguliwe kuwa mbunge katika kipindi cha tatu cha uongozi wangu ," na tunaendelea na tumejipanga kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi ili 2020 kusiwe na maswali mengi"alifafanua Dk.Kawambwa.

Hata hivyo Dk.Kawambwa amewezesha vikundi vya ujasiriamali 26 kiasi cha sh. mil.15.400 kupitia mfuko wa jimbo ili kuviinua kimaendeleo.

Mbali na hayo mbunge huyo alichangia mifuko ,1000 ya saruji ambayo ilipelekwa katika kata 11 zilizopo jimboni hapo ,ambapo kila kata ilipatiwa mifuko kati ya 100-150.

Nae Mwenyekit wa CCM Kata ya Nianjema Salum Mikugo, alisema lengo kubwa la kamati ya siasa kutembelea miradi ya maendeleo ni kujiridhisha kwa kujionea kwa macho pasipo kupelekewa ofisini.

Alisema huu ni wakati wa kufanya kazi kwa kufikia miradi hiyo na wamedhamiria kufanya kazi ya CCM na kuisimamia serikali ,ilani ya Chama.

"Kikubwa zaidi ni kuleta imani kwa wananchi na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi ili kuondoa upenyo kwa wapinzani ," alisema Mikugo .

Mikugo alisema wanaendelea kusimamia ilani ili kuishauri serikali pale panapohitajika hatimae kuvuka hatua kimaendeleo kwenye kata.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Nianjema Abdul Pialla,alisema zoezi la uhakiki wa mpango wa malipo ya matokeo ya ufanisi wa kazi (RBF)ili kuboresha huduma za afya lilibaini mapungufu kwenye zahanati ya Kimara Ng'ombe uliosababisha halmashauri kushindwa kutoa ahadi yake ya mil.kumi.

Alisema alifanya mazungumzo na mganga mkuu wa wilaya ya Bagamoyo na kuambiwa  liongezwe eneo la zahanati litakalofikia hekari moja.

Pialla aliomba wataalamu kujenga ushirikiano na viongozi wa kata na serikali za vitongoji hali itakayosaidia kujua kinachoendelea ili waweze kuwa na majibu kwa  wananchi.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Kimara Ng'ombe Yusuph Mbagala,alieleza ujenzi wa zahanati ya Kipara Ng'ombe ulinza kujengwa mwaka 2013 baada ya kuona umuhimu wa kujengwa kwa zahanati hiyo.

Alisema kukosekana kwa zahanati katika eneo hilo kunasababisha wananchi kufuata huduma za kiafya hospital ya wilaya ambako ni mbali na kusababisha ongezeko la gharama za matibabu ambazo wanashindwa kuzimudu.

Mbagala alisema kuna changamoto zilizojitokeza katika ujenzi huo ikiwa ni pamoja na wananchi kukata tamaa kutokana na halmashauri  ya Bagamoyo kuchelewa kutekeleza ahadi ya sh.mil.kumi ambayo haijatekelezwa.

Alisema hali hiyo inarudisha nyuma juhudi za wananchi na waliojitokeza kuwaunga mkono katika ujenzi huo.
MBUNGE wa jimbo la Bagamoyo, Dk.Shukuru Kawambwa wa tatu kushoto mwenye kitambaa kichwani akiwa ameambatana na kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi ya CCM ya kata ya Nianjema, kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika ziara yake ya siku moja kwenye kata hiyo,wa pili kushoto mwenye kibagharashia ni Mwenyekit wa Ccm Nianjema Salum Mikugo .
(Picha na Mwamvua Mwinyi)

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages