DK.Kalemani -Nguzo za umeme za zege zitumike ili kuimarisha miradi ya umeme - Mtazamo News
Tangaza Biashara yako Hapa +255755 300 337

HABARI ZA HIVI PUNDE

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Wednesday, 22 November 2017

DK.Kalemani -Nguzo za umeme za zege zitumike ili kuimarisha miradi ya umeme

 Waziri wa Nishati Dk .Merdard Kalemani ,akizungumza na baadhi ya wananchi,viongozi na wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha East Africa Infrastructure Engineering  Ltd kilichopo Fukayosi wilayani Bagamoyo,mkoani Bagamoyo,wakati alipotembelea kiwanda hicho kujionea uzalishaji wa nguzo hizo.(picha na Mwamvua Mwinyi)
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

KIWANDA cha kutengeneza nguzo za umeme za zege cha East Africa Infrastructure Engineering  Ltd kilichopo Fukayosi wilayani Bagamoyo,mkoani Pwani ,kimeanza uzalishaji nguzo hizo zinazodumu kwa zaidi ya miaka 70 hivyo kupunguza gharama za kubadili nguzo nyingine kama ilivyo kwa nguzo zilizozoeleka za miti.

Kutokana na teknolojia hiyo ya kisasa serikali imelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuanza kutumia nguzo hizo kwenye miradi mikubwa ikiwemo ule wa Stieglers Gorge unaotarajiwa kujengwa kwenye maporomoko ya mto Rufiji.

Waziri wa Nishati Dk .Merdard Kalemani aliyasema hayo wakati alipotembelea kiwanda hicho wilayani Bagamoyo kujionea uzalishaji wa nguzo hizo.

Alieleza baada ya serikali kupiga marufuku uingizwaji wa nguzo za umeme toka nchi za nje na kuruhusu wawekezaji kutengeneza nchini sasa umefika wakati TANESCO ianze kutumia nguzo za zege kuanzia Desemba mwaka huu kwenye miradi mikubwa.

Dk.Kalemani alisema mara utakapokamilika mradi wa Stieglers Gorge utaweza kuzalisha megawati 2,100 ikiwa ni uzalishaji wa megawati nyingi tangu kipindi cha mwaka 1930 uzalishaji ulipokuwa megawati 1,451 hadi sasa.

Aidha ifikapo Agosti 2018 nchi itaweza kuzalisha megawati 240 kutoka kwenye mradi wa chanzo cha umeme cha Kinyerezi namba mbili ambapo kuanzia Desemba mwaka huu megawati 30 zitakuwa zinaunganishwa kwenye greti ya Taifa kupitia mradi huo .

Dk.Kalemani alielezea kwamba,kadri megawati za umeme zinavyozidi kuongezeka kwenye uzalishaji mbalimbali wa miradi ya umeme inayojengwa itatosheleza hasa kwenye viwanda .

“Mradi huo unatarajia kutumia nguzo kati ya 500 hadi 600 na kutokana na ukubwa wake  lazima tutumie nguzo imara ambazo zinauwezo wa kudumu kwa miaka 70 kuliko kutumia nguzo za miti ambazo zinadumu kwa miaka mitatu”

“Utumiaji wa nguzo zinazotumia miti madhara ni kuharibu vyanzo vya maji na mazingira hivyo kaeni na kampuni hii mshirikiane ili mradi wa Rufiji utakapoanza kutekelezwa zitumike nguzo za zege ambapo kilometa 36 zitatumia nguzo hizo”
“Maeneo ya mbugani huwezi kutumia nguzo za miti ama kupitisha umeme chini ya ardhi kwani lengo langu ni kuhakikisha kila mwananchi anapata umeme,”

“Mmetekeleza agizo la serikali la awamu ya tano kuanzisha viwanda vyetu kwa kutengeneza malighafi zitakazotusaidia wenyewe na kuokoa fedha za kununua malighafi kutoka nje,” Huwezi kuimarisha uchumi wa viwanda kwa kutegemea malighafi toka nje ya nchi ,” alisema Dk Kalemani.

Dk.Kalemani alisema walipozuia nguzo zisitoke nje kulikuwa na watu 29,000 walikuwa hawajaunganishiwa umeme lakini baada ya hapo watu 20,000 waliunganishiwa umeme .

Alibainisha kama kuna mteja hajaunganishiwa umeme zaidi ya mwezi meneja hajafanya hivyo  atachukuliwa hatua kwani changamoto ya kuchelewesha kuunganishiwa hilo ni tatizo la meneja husika.

Akielezea juu ya kiwanda hicho mmiliki -Otieno Igogo ambae anashirikiana na Wachina katika uzalishaji wa nguzo hizo alisema kwasasa wanazalisha nguzo 50 kwa siku huku wakiwa wameajili watu 70.
Alisema endapo zege hizo zitatumiwa itapunguza gharama za kuweka nyingine kama ilivyo kwa zile za miti.

Igogo alisema kuwa gharama za ujenzi wa kiwanda hicho ni kiasi cha shilingi  bilioni 13 ambapo changamoto inayowakabili ni kukosa soko kwenye sekta za umma na binafsi na kuiomba serikali kuwaunga mkono .

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa mkoa  wa Pwani,mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Majid Mwanga ,alimshukuru Waziri wa Nishati kwa kuendelea kufanikisha upatikanaji wa umeme hasa ikizingatiwa mkoa huo ni moja ya mikoa yenye viwanda vingi hapa nchini.

Alieleza wilaya ya Bagamoyo na mkoa una mahitaji makubwa ya umeme kutokana na kuwa na uwekezaji mkubwa hasa kwenye sekta ya viwanda ambayo ina mahitaji makubwa ya umeme .

Mwanga alielezea mipango mbalimbali ya uzalishaji umeme itasaidia kuondoa tatizo la upungufu wa umeme.

Akishukuru kwa niaba ya wananchi wa Bagamoyo Mbunge wa Jimbo hilo Dk Shukuru  Kawambwa alisema utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme ukiwemo ule wa REA ni miradi muhimu ambayo inakwenda kuondoa tatizo la umeme.

Dk Kawambwa alimpongeza Rais wa awamu ya tano Dk John Magufuli kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji wa umeme ambapo kwa miaka mingi kumekuwa na upungufu wa umeme na baadhi ya maeneo kutokuwa na huduma hiyo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages