Header Ads


Ummy Mwalimu Aagiza Vituo vya Afya na Hospitali zote za Serikali kutenga siku maalum kila mwezi kwa ajili ya kupima Saratani ya Matiti na ya Mlango wa Kizazi

Asema asilimia 45 ya wagonjwa wa Saratani nchini ni wanawake wanaougua
Saratani ya Matiti na ya Mlango wa Kizazi.

Asilimia 80 ya wagonjwa hawa hufika Hospitalini ugonjwa ukiwa hatua za mwisho.

Aweka lengo la kuchunguza wanawake milioni 3 nchi nzima ifikapo Desemba 2018.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu ametumia mamlaka aliyonayo kuagiza Vituo vya Afya (Health Centres) na Hospitali zote za Serikali nchini kutenga Siku moja kila mwezi kwa ajili ya kuwapima wanawake Saratani  ya Matiti na ya Mlango wa Kizazi ili kuwezesha ugunduzi wa mapema wa saratani na hivyo kuokoa maisha ya wanawake hasa wa vijijini na wa kipato cha chini.

Mhe Ummy ametoa agizo hilo leo katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es salaam wakati wa kukamilisha Matembezi ya kuhamasisha wanawake kupima Saratani ya Matiti. Octoba kila mwaka, jumuiya ya kimataifa hutumia mwezi huu kuhamasisha upimaji wa Saratani ya Matiti.

Mhe Ummy ameeleza kuwa Saratani inazidi kutafuna maisha ya watanzania hasa wa kipato cha chini. Na idadi ya wagonjwa na vifo itaongezeka mara mbili ifikapo mwaka 2020 endapo Serikali,  wadau  na wananchi hawatachukua hatua zaidi za kupambana na ugonjwa huu. 

"Kinachoniumiza zaidi ni kuona kuwa asilimia 80 ya  wagonjwa wote wanaofika Hospitalini kupata huduma za matibabu ya  Saratani nchini wengi wakiwa ni wanawake wenzangu hufika ugonjwa ukiwa katika hatua za mwisho za  ugonjwa na hivyo kufanya matokeo ya matibabu kutokuwa mazuri" alisema mhe Ummy. 

Saratanizinazoongoza hapa nchini ni; Saratani ya mlango wa kizazi (34%), Saratani ya Ngozi (kaporsis Sarcoma)(13%), Saratani ya matiti (12%), Saratani ya mfumo wa njia ya chakula (10%), Saratani ya Kichwa na shingo (7%), Saratani ya Matezi (6%), Saratani ya Damu (4%), Saratani ya Kibofu cha mkojo (3%),Saratani ya ngozi (3%), Saratani ya Macho (2%), na saratani ya tezi dume (2%). 

Mhe Ummy ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Mhe Dr John Pombe Magufuli imedhamiria kuhakikisha wananchi wanapata huduma za uchunguzi na matibabu ya Saratani kwa urahisi, haraka na bila malipo yoyote. *Hivyo, Serikali imeongeza Bajeti ya Dawa za Saratani kutoka shs milioni 700 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi bilioni 7 mwaka 2017. 


Na kwa kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wa Saratani ni wanawake, mhe Ummy ameeleza kuwa mwaka huu 2017, *Serikali kupitia Wizara ya Afya imeongeza Vituo vya Uchunguzi na Matibabu ya Awali ya Saratani katika Vituo vinavyomilikiwa na Serikali kutoka 343 mwaka 2016 hadi 443 mwaka 2017.

Lengo la hatua hii ni kuhakikisha wanawake wenye saratani wanagunduliwa mapema ili waweze kupata huduma za matibabu na kupona kabisa. Mhe Ummy amesema amejiwekea lengo la kuhakikisha wanawake milioni 3 nchini wanafikiwa na huduma za uchunguzi wa Saratani ya Matiti na ya Mlango wa Kizazi ifikapo Desemba 2018.* Hivyo, amewataka wanawake kujitokeza kupima. 

Na kila Mkoa kujiwekea lengo la kupima angalau asilimia 20 ya wanawake wa umri wa kuzaa (miaka 15 - 49) katika mikoa yao. Saratani Inatibika endapo itagunduliwa mapema! Wakati ni Sasa! Tunao wajibu wa kuokoa maisha! Alisema mhe Ummy.
Post a Comment
Powered by Blogger.