Naibu Waziri Kwandikwa amwagiza Chico kujenga kiwanja cha ndege Shinyanga. - Mtazamo News
Tangaza Biashara yako Hapa +255755 300 337

HABARI ZA HIVI PUNDE

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Thursday, 19 October 2017

Naibu Waziri Kwandikwa amwagiza Chico kujenga kiwanja cha ndege Shinyanga.


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, akizungumza na wananchi wa Mwigumbi mkoani Shinyanga, alipofanya ziara ya kukagua barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3), inayounganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.
     Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, akifafanua jambo kwa Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Bi. Josephine Matiro (Watatu kushoto), alipofika mkoani humo kukagua  maendeleo ya kiwanja cha ndege cha Shinyanga kilichopo eneo la Ibadakuli.      
 Meneja wa Kiwanja cha Ndege cha Shinyanga, Bw. Julius Misollow, akitoa taarifa ya maendeleo ya kiwanja hicho kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, alipofika kiwanjani hapo kujionea maendeleo yake.
 Muonekano wa kiwanja cha Ndege cha Shinyanga ambacho kinatatrajiwa kujengwa kwa kiwango cha lami na Mkandarasi wa Kampuni ya ujenzi ya kichina ya CHICO.
 Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), mkoani Simiyu, Mhandisi Albert Kent, akimuonesha Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, kazi za ujenzi zinazoendelea katika barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3).
 Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhe. Elius Kwandikwa, akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya kichina ya CHICO alipokuwa akikagua barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3) inayounganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.

Muonekano wa Barabara ya Mwigumbi – Maswa (KM 50.3), inayojengwa kwa kiwango cha lami  na mkandarasi CHICO kutoka nchini China. Barabara hii inaunganisha mkoa wa Shinyanga na Simiyu.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mheshimiwa Elius Kwandikwa, amemtaka Mkandarasi wa kampuni ya ujenzi ya kichina ya CHICO aliyepewa zabuni ya ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Shinyanga kufika eneo la mradi na kuanza ujenzi wa kiwanja hicho haraka iwezekanavyo.
Akizungumza mara baada ya kukagua maendeleo
ya kiwanja hicho katika eneo la Ibadakuli leo, mkoani Shinyanga, Naibu
Waziri Kwandikwa, amesema kuwa haoni sababu ya mkandarasi huyo kuchelewa kuleta
vifaa vyake katika eneo la mradi hadi sasa wakati tayari mkataba wa kuanza kazi
hiyo umeshasainiwa.

"Mkandarasi hana sababu ya kuchelewa
kuanza kazi wakati fedha zipo na zimeshatengwa kwa ajili ya mradi huu na
mkataba umeshasainiwa,  sasa namwagiza mkandarasi huyu kuleta vifaa vyake
na kuanza kazi mara moja", amesema Naibu Waziri Kwandikwa.

Aidha, Naibu Waziri huyo amemtaka
Meneja wa kiwanja hicho kuhakikisha anatoa ushirikiano na kumsimamia mkandarasi
huyo ili kuhakikisha kiwanja hicho kinakamilika mapema nakwa viwango
vinavyotakiwa.

"Naamini tukimsimamia vizuri mkandarasi
huyu tutapata kiwanja kizuri na imara hapa Shinyanga na tutafungua fursa
mbalimbali za kiuchumi katika mkoa huu", amesisitiza Naibu Waziri
Kwandikwa.

Kwa upande wake, Meneja wa kiwanja cha ndege
cha Shinyanga, Julius Misollow, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kutoa
ushirikiano kwa mkandarasi huyo atakapowasili eneo la mradi.

Amefafanua kuwa mradi huo unatarajiwa kuhusisha
ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege, jengo la abiria, maeneo ya
maegesho ya ndege na mnara wa kuongozea ndege.

Ameongeza kuwa ujenzi wa kiwanja
hicho kwa kiwango cha lami chenye urefu wa kilomita mbili unatarajiwa kugharimu
zaidi ya shilingi Bilioni 49.

Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kwandikwa,
amekagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya Mwigumbi - Maswa (KM 50.3), mkoani
Simiyu na kumsisitiza mkandarasi anayejenga barabara hiyo kuikamilisha kwa
wakati na kwa viwango.

Amesisitiza kuwa kukamilika kwa
barabara hiyo ambayo ni kiungo kwa wananchi wa Maswa, Bariadi, Lamadi na
Mwanza, kutarahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika maeneo
hayo.

Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS), mkoani Simiyu, Mhandisi Albert Kent, amesema kuwa mradi upo katika
hatua nzuri na unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili kutoka sasa.

Naibu Waziri Kwandikwa amefanya ziara ya kikazi
katika mkoa wa Shinyanga na Simiyu ambapo amekagua miradi mbalimbali
inayotekelezwa na Wizara yake.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages