Habari za sasa hivi

WANANCHI WATAKIWA KULIPA KODI YA PANGO LA ARDHI KWA WAKATI - MBEYA

Msafiri Mmassy kutoka Ofisi ya Kamishna msaidizi nyanda za juu Kusini Magharibi akieleza umuhimu wa kulipa kodi ya pango la Ardhi kwa waandishi wa habari (hawako pichani) akiwa na Shenya Magori.

Ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda ya nyanda za juu Kusini imekusanya jumla ya Tsh. 5.8 bilioni kodi ya pango la ardhi kwa kipindi cha  kuanzi Julai 2016 hadi mei 2017 ikishirikiana na Halmashauri 34 zilizopo katika Kanda.

Makusanyo hayo yameongezeka baada ya kusambaza hati za madai kwa wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi 51 na kuwafikisha mahakamani. Jumla ya Tsh. 1.2 bilioni imekusanywa kutoka kwa baadhi ya wadaiwa waliofikishwa mahakani na hivyo kufanya makusanyo hayo kuongezeka.

Pamoja na hatua hizo za kuwafikisha wadaiwa sugu mahakamani, ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi nyanda za juu Kusini imetoa rai kwa wadaiwa wote wa kodi ya pango la ardhi kulipa kodi kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni.

Kodi ya pango la ardhi hulipwa kila mwaka kuanzia tarehe 01 Julai hadi tarehe 31 Disemba bila tozo. Endapo kodi hii haitalipwa kwa wakati, kuanzia tarehe 01 Januari italipwa na tozo ya asilimia moja (1%) ya kodi husika.

Ni vyema wananchi wakatambua kwamba, Ardhi yote ya Tanzani ni mali ya Umma na msimamizi ni Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania. Hivyo, wananchi ni wapangaji wa ardhi na wanamiliki kwa mkataba wa miaka 33, 66 au 99 ambao ni Hati miliki ya kiwanja husika.

Kipengele cha kwanza kabisa cha Hati miliki kimeeleza masharti mbalimbali ya umiliki wa ardhi. Mojawapo ni kulipa kodi ya pango la ardhi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu. Kodi hiyo italipwa kulingana na ukubwa wa kiwanja, matumizi yake pamoja na eneo kiwanja kilipo.

Kutokulipa kodi ya Pango la Ardhi ni kosa kisheria. Adhabu inayoweza kuchukuliwa kwa kosa hili pamoja na kupelekwa mahakamani ni kukamatiwa mali au kufutiwa umiliki. Kodi ya pango la ardhi ni kwa kwa maendeleo ya taifa letu hivyo, hatuna budi kulipa kwa wakati ili kuepuka usumbufu.