YANGA INAHITAJI ALAMA 3 KUTANGAZA UBINGWA KWA MARA YA TATU MFULULIZO - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka
Advertise Here +255755 300 337

HEADLINES

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Sunday, 14 May 2017

YANGA INAHITAJI ALAMA 3 KUTANGAZA UBINGWA KWA MARA YA TATU MFULULIZO

Mabingwa watetezi  Yanga  wamerudi kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kutokana na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City ya Mbeya jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo unawafanya mabingwa hao watetezi watimize pointi 65 baada ya kucheza mechi 28 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu. Simba inaangukia nafasi ya pili kwa pointi zake 65 za mechi 29, ikizidiwa wastani wa mabao.  

Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Andrew Shamba wa Pwani, aliyesaidiwa na Joseph Pombe wa Shinyanga na Haji Mwalukuta wa Tanga, dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika Yanga ikiwa inaongoza 1-0.


Bao hilo lilifungwa na winga Simon Happygod Msuva kwa kichwa dakika ya saba tu akimalizia krosi ya Hassan Kessy.

Hata hivyo, Msuva hakuweza kushangilia bao hilo, kwani wakati anaenda hewani kuunganisha krosi ya Niyonzima aligongana na beki wa Mbeya City, Tumba Lui na kuchanika juu ya jicho la kulia.

Msuva hakuweza kuendelea na mchezo na kupelekwa kwenye zahanati ndogo ya Uwanja wa Taifa kwa matibabu zaidi nafasi yake ikichukuliwa na beki Juma Abdul.

Kwa mabadiliko hayo, Kessy alikwenda kucheza kama winga wa kulia na Abdul akacheza beki ya kulia, ingawa walikuwa wakipokezana kuzuia na kushambulia. 

Kipindi cha pili Mbeya City walikianza vizuri na kufanikiwa kupata bao la kusawazisha lililofungwa na beki wake wa kulia, Haruna Shamte dakika ya 57 akitumia mwanya wa mabeki wa Yanga kupoteana.

Hata hivyo, Yanga wakafanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa dakika ya 64 akimalizia mpira wa adhabu wa Juma Abdul.

Mbeya City ilijitahidi kujaribu kusawazisha bao hilo, lakini tayari wapinzani wao, Yanga walikuwa wamekwishaanza kucheza kwa kujihami zaidi na kushambulia kwa kushitukiza.

Mrisho Ngassa aliingia kipindi cha pili upande wa Mbeya City, lakini hakuwa na madhara kwa timu ya timu yake ya zamani zaidi tu ya kusisimua mashabiki kwa uchezaji wake mzuri.


Matokeo mengine ya mechi zilizochezwa leo

Kagera Sugar 2-1 Mbao FC

JKT Ruvu 0-1 Majimaji

Tanzania Prisons 2-1 Ndanda FC


Mtibwa Sugar 4 -2 Mwadui FC

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages