SERIKALI YAKUSANYA MRABAHA DOLA 158,093 MNADA WA TANZANITE - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka
Advertise Here +255755 300 337

HEADLINES

Post Top Ad

Advertise Here +255755 300 337

Tuesday, 9 May 2017

SERIKALI YAKUSANYA MRABAHA DOLA 158,093 MNADA WA TANZANITE

Rhoda James na Asteria Muhozya, Arusha
Serikali kupitia Mnada wa Madini ya Tanzanite imekusanya Mrabaha wa Dola za Marekani 158,093 sawa na shilingi 347,804,600 kati ya hizo, Halmashauri ya Wilaya ya Simajiro italipwa shilingi 20,868,276 kama kodi ya Huduma.

Hayo yalibainishwa na Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka wakati   wa kutangaza washindi wa mnada wa madini ya Tanzanite katika Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya Madini ya Vito ya Arusha yaliyofanyika jijini humo kuanzia tarehe 3-5 Mei, 2017.

Kamishna Mchwampaka alisema kuwa, Madini hayo ya Tanzanite yaliyouzwa katika mnada huo yalikuwa ni jumla ya gramu 691,060.33 na kuongeza kuwa, yaliuzwa kwa Dola za Marekani 3,161,860 sawa na asilimia 100 ya madini yote yaliyowasilishwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uthaminishaji wa Madini ya Almas (TANSORT) Wizara ya Nishati na Madini, Archard Kalugendo akitangaza washindi, alizitaja kampuni za Nova Summit Internatinal Ltd na Viber Global International Ltd kuwa washindi wa mnada huo.

“Miongoni mwa kampuni zilizoshinda mnada ni pamoja na kampuni ya Kitanzania ya Godi Mwanga and Family Ltd. Hii ni ishara nzuri kwa Tanzania na ninawasihi wadau wengine wa madini nchini kujitokeza. Mnada wa tanzanite ulikuwa wa wazi na aliye bid kwa kiasi kikubwa ndiye aliyeshinda,” alisema Kalugendo.

Kwa upande wake, Waziri  wa Madini na Maendeleo ya Biashara na Nigeria, Abubakar Bwari, ambaye aliongoza ujumbe wa Serikali ya Nigeria kushiriki maonesho hayo, alitoa pongezi kwa Tanzania kwa kuendelea kudumisha amani iliyopo nchini ikiwemo kupongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutangaza madini ya Tanzanite pamoja na kuendeleza sekta ya madini.

Akizungumzia Sekta ya Madini ya Nigeria, alisema kuwa hivi sasa nchi hiyo inaweka nguvu katika shughuli za madini na kilimo ili kuhakikisha kuwa, rasilimali hizo zinalinufaisha taifa hilo.

Aliongeza kuwa, imeshiriki maonesho hayo ili kujifunza namna Tanzania inavyoongeza thamani madini yake na kuongeza kuwa, iko tayari kujifunza kutoka Tanzania na kueleza kuwa, hivi karibuni nchi yake itatoa ushindani kwa Tanzania kupitia Maonesho ya Kimataifa ya Vito hususan katika suala la Uthaminishaji wa Madini ya Vito.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo akifunga maonesho hayo aliishukuru Kamati ya Maonesho ya Madini ya Vito ya Arusha (AGF) kwa kuratibu vema zoezi hilo.
Gambo alisema kuwa, pamoja na changamoto zilizopo kwa upande wa Serikali na Chama cha Wafanyabiashara wa Madini (TAMIDA) bado Serikali inafaidika kutokana na Maonesho hayo.

“Madini ya vito hususan Tanzanite ikiuzwa Serikali inapata mrabaha na Halmashauri inapata Kodi ya Huduma, pia jiji la Arusha linapata faida nyingi zikiwemo matumizi ya Hotel, kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Arusha kama vile Mlima Kilimajaro, Bonde la Ufa la Ngorongoro na kadhalika,”.

Alitoa wito kwa Wizara ya Nishati na Madini kushirikiana na Wafanyabiashara kwa karibu ili kupunguza urasimu uliopo na pia kushiriki katika kutatua changamoto zilizopo baina yao.

Pia, alisema kuwa, ni wakati sasa wa Serikali kuhakikisha kuwa angalau kwa kipindi cha ndani ya Miaka miwili madini ghafi hayauzwi nje badala yake yanaongezwa Thamani nchini, kwa kuwa suala hilo litawezesha kupanua wigo wa ajira na kukuza uchumi wa nchi.

Pia alitoa wito kwa wafanyabiashara wote wa madini nchini kushiriki, kwenye Maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka kikamilifu kulipa kodi.
 Vilevile, Gambo aliwapongeza wauzaji wa madini wa kati (madalali) kwa kushiriki Maonesho hayo kwa mara ya kwanza.

“Hata kama haukuuza kwa kipindi hiki, lakini faida ni nyingi kwa kuwa mmejenga mtandao wa kibiashara na kampuni kubwa duniani na pia kukutana na wafanyabiashara wakubwa” alisema Gambo.

Maonesho ya 6 ya Kimataifa ya madini ya vito yalifunguliwa rasmi tarehe 3 Mei na Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Joel bendera na kufungwa tarehe 5 Mei, 2017 na Mkuu wa Mkoa Arusha Mrisho Gambo.


 Nchi za nje zilizoshiriki maonesho hayo ni pamoja na pamoja na USA, India, Isreal, China, Japan, Uswisi na Ujerumani pamoja na makapuni 49 ya ndani na nje ambayo pia yalishiriki.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad


Pages