Habari za sasa hivi

NDIKILO-ATANGAZA KIAMA KWA WANAOTUMIA VIBAYA BANDARI BUBU/WASAFIRISHAJI WAHAMIAJI HARAMU

 Mkuu wa Mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo ,akizungumza.

Na Mwamvua Mwinyi,Pwani

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amewaonya watu wanaojihusisha na biashara ya usafirishaji wa wahamiaji haramu pamoja na wale wanaopitisha magendo kupitia bandari bubu na njia nyingine za panya.

Aidha amesema kwasasa wamedhibiti mchezo uliokuwa ukifanywa na baadhi ya watu, waliokuwa wakipitisha aina mbalimbali za madawa ya kulevya ikiwemo bangi wakijidai wanapitisha madumu ya mafuta .

Hata hivyo mkuu huyo wa mkoa huo,ametangazia kiama wale wote wanaofanya biashara hizo na kusisitiza Pwani sio lango la magendo kama wanavyodhania .

Akizungumzia masuala hayo mkoani hapo,mhandisi Ndikilo alieleza ,wilaya ya Bagamoyo ina jumla ya bandari bubu 19 ambazo raia wasio wema wanazitumia vibaya hivyo kusababisha kukosa mapato.

Alisema wapo wafanyabiashara wanaoingiza na kupitisha bidhaa zao pasipo kulipia kodi ama ushuru na kushindwa kuingiza mapato ya halmashauri husika,wilaya na mkoa kijumla.

“Mtu anapitisha madumu ya mafuta 2,000 na kati yake 1,000 ameweka bangi ama madawa ya kulevya ya aina nyingine,hii haikubaliki ,kwasasa tunawadhibiti na atakaebainika ni lazima atiwe nguvuni”alisema mhandisi Ndikilo.

Mhandisi Ndikilo,alielezea kwamba,moja ya eneo linalotumika vibaya ni Saadan hivyo ameomba itumike vizuri ili kuleta mapato makubwa.

Alisema  mwambao huo umepitiwa na bahari ya hindi ikiwa ni pamoja na Kibiti,Bagamoyo ,Mkuranga na Rufiji ambapo kunaingiza wahamiaji haramu,silaha ,watu waharifu na magendo mbalimbali.

 “Hivi karibuni tulifanya mkutano wa wakuu wa mikoa ,mkutano ambao ulifanyika Zanzibar,na mikakati iliwekwa ikiwemo Saadan kulasimishwa “
Mhandisi Ndikilo,alisema kuanzia sasa Saadan itakuwa inatambulika na mamlaka ya bandari Tanzania sanjali na Bagamoyo,Nyamisati na Kisiju .

"Hatua hiyo ya kulasimishwa ,itasaidia kutambulika ili kuondoa uchochoro na njia za panya ambazo zilikuwa zikididimiza mapato ya ndani kutokana na kuingiza na kupitisha bidhaa mbalimbali kinyemela".

"Pia wale waliokuwa wakijihusisha na kupitisha madawa ya kulevya hasa bangi,mirungi kuwakomesha kwa kushindwa kupata mianya ya kupitisha madawa hayo"alisema.

Alieleza, usafirishaji wa wahamiaji haramu hauna nafasi mkoani Pwani,kwani atakaebainika kupitisha wahamiaji hao mkoani humo atakiona.

Wakati huo huo, mhandisi Ndikilo,alisema wilaya ya Bagamoyo pekee ndani ya miezi sita wamekamata wahamiaji haramu zaidi ya 411 ,suala ambalo likifumbiwa macho litaleta athari .

Nae mwenyekiti wa halmashauri ya Chalinze,Said Zikatimu, alisema wanaongeza wakusanyaji na wasimamizi kizuizi cha Saadan ambako wamegundua mkaa mwingi unatoroshwa na kupelekwa Zanzibar hivyo wanapambana ili usivushwe .

Alifafanua,changamoto kubwa ni halmashauri hiyo kuwa kubwa na kugawanyika hivyo wakwepa kodi na ushuru kutumia kigezo hicho .
Zikatimu alisema kutokana na hilo wameongeza nguvu eneo la Gongo na Miono.