28 APRILI 2017 - RAIS DKT.MAGUFULI APOKEA TAARIFA YA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI WA UMMA - Mtazamo News-Habari Bila Mipaka

Breaking

Tangaza nasi Hapa-+255787 942 222

Post Top Ad

Post Top Ad


Saturday, 29 April 2017

28 APRILI 2017 - RAIS DKT.MAGUFULI APOKEA TAARIFA YA ZOEZI LA UHAKIKI WA VYETI KWA WATUMISHI WA UMMA

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 28 Aprili 2017, amepokea taarifa ya uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma katika ukumbi wa Chimwaga mkoani Dodoma na kuiagiza Wizara ya fedha kuwaondoa katika orodha ya Watumishi wa Umma na kusimamisha mishahara ya Watumishi 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya kugushi.

Idadi ya watumishi hao imebainika baada ya Waziri wa  Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Angela Kairuki kukabidhi taarifa ya zoezi la uhakiki wa vyeti kwa watumishi wa Umma zaidi ya laki nne kwa Rais Magufuli, zoezi ambalo liliendeshwa na Serikali kuanzia mwezi Oktoba mwaka 2016.

Rais Magufuli pia amewataka Watumishi 9,932 waliobainika kutumia vyeti vya kugushi kujiondoa wenyewe katika utumishi wa Umma kabla ya tarehe 15 Mei 2017 na baada ya muda huo hatua za kisheria zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

'' Kwa hiyo Waziri Mkuu upo hapa na Waheshimiwa Mawaziri wote mnaohusika, hawa watu 9932 mshahara wao wa mwezi huu ukatwe na waondoke mara moja kwenye Utumishi wa Umma kuanzia leo, watakao baki mpaka tukiingia mwezi wa tano tuwapeleke kwa mujibu wa sheria ili kusudi wakafungwe hiyo miaka saba'' amesema Rais Magufuli.

Pia Rais Magufuli ameiagiza Wizara ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora kutangaza nafasi hizo 9,932 upya ili wenye sifa stahiki waweze kuomba
Aidha, Rais Magufuli ameiagiza Tume inayofanya uhakiki wa vyeti kwa Watumishi wa Umma kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu kuendelea na uchunguzi wa  Watumishi wa Umma 1538 waliobainika kutumia vyeti vyenye utata hadi Mei 15, 2017

'' hawa wenye vyeti vya utata kwa maana kuwa vyeti vyao  vinatumiwa na watu zaidi ya mmoja, Wizara ya Utumishi muhakikishe kufika tarehe 15 muwe mmeshajua ni nani mwenye cheti chake, na mshahara wa mwezi huu wasipewe kwanza mpaka atakayepatikana mwenye cheti halali'' amesema Rais Magufuli.

Pia ameagiza uchunguzi ufanyike kwa watumishi 11,596 wenye vyeti vya Utaalumu bila kuwasilisha vyeti vya kidato na Sita kwa kuwa sio fani zote zinazohitaji kuwa na vyeti vya kidato cha Sita ili kusomea utaalamu husika na kuagiza kulipwa mishahara yao kama kawaida.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amezindua maadhimisho ya miaka kumi tangu kuanzishwa kwa Chuo kikuu cha Dodoma.

Rais magufuli amewaelezea Wanajumuiya ya Chuo Kikuu cha Dodoma mipango mbalimbali inayofanywa na Serikali  katika kuboresha maisha ya Watanzania na kukuza Uchumi ikiwa ni pamoja na kuimarisha Miundombinu ya Usafiri kwa kununua ndege mpya Sita na Ujenzi wa Reli ya kisasa.

Mheshimiwa Rais amesema hatua ya Serikali kuimarisha huduma za jamii inatokana na mafanikio ya Serikali kudhibiti upotevu wa mapato na hivyo kuwataka wananchi kuunga mkono jitihada za Serikali ili kukamilisha malengo ya Tanzania ya viwanda.

Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Chamwino, Dodoma

28 Aprili, 2017

No comments:

Post Top Ad

Tangaza nasi Hapa-+255787 942 222